Novena ni mtiririko wa sala za siku tisa, huwa ni sala zenye dhumuni au nia maalum au mara nyingine huwa ni kwa ajili ya shukrani.
Neno novena lilitokana na neno la kilatin "novem" likimaanisha "tisa". Na hizi siku tisa zinaashiria siku tisa ambazo mitume na mama Bikira Maria walikaa pamoja ndani, yaani tangu Yesu alipopaa mbinguni hadi siku ya pentekoste (Mdo 1:14)
🙏 MAMBO YA KUZINGATIA UNAPOTAKA KUSALI NOVENA.
1. Kujua maana ya novena, kama nilivyokwisha eleza hapo juu.
2. Kutambua kwamba novena si sala ya muujiza, bali ni sala kwa ajili ya nia maalumu. Kwa hiyo si lazma muujiza utokee.
3. Jiulize kwanin unataka kusali novena. Hapa unapaswa kujua nia yako ya kusali novena.
4. Dhamiria kusali novena kwa Imani na matumaini yote kwamba unachoomba utapata. Weka Imani yako kwa Mungu.
5. Zingatia kuwa novena ni tendo la ibada, kwa hiyo maandalizi mengine ya kiroho ni muhimu, kama vile toba, kuungama, kufunga, kutoa sadaka, kutafakari n.k.
6. Dhamiria kumaliza vema siku zote tisa za novena. Maana ukiruka siku moja tu unakuwa umeharibu novena nzima.
🙏 JINSI YA KUSALI NOVENA.
1. Uwe umejiandaa vizuri kiroho.
2. Uwe umeshachagua sala ya novena utakayotumia, maana zipo nyingi. Mfano novena ya Mt. Yuda Thadei n.k.
3. Uwe na nia maalum kwa ajili ya novena husika.
4. Uwe unajua siku ya kuanza novena, pamoja na saa ya kusali. Maana novena inapaswa kusaliwa muda mmoja kila siku.
5. Sali mara moja tu kwa siku, kwa siku zote tisa.
6. Wakati wa kusali usisahau kukazia nia yako ya novena. Mawazo yako yote yawe kwenye nia moja.
7. Sali katika eneo tulivu, ili mawazo yako yawe sehemu moja.
🙏 HATUA ZA KUSALI NOVENA.
1. Kama kawaida unaanza na ishara ya msalaba.
2. Sala za kawaida, hasa sala za toba, sala za Roho Mtakatifu n.k.
3. Tafakari kidogo kuhusu ukuu wa Mungu na iweke nia yako mbele ya Mungu.
4. Sali novena yako, kwa ibada, utulivu, imani na matumaini.
5. Sala za shukrani, pamoja na sala nyingine.